Katika utamaduni wa Kiyahudi, ukoo unarudi nyuma hadi kwa mababu wa Biblia kama vile Abrahamu, Isaka, Yakobo na wanae 12 katika milenia ya 2 KK. Lakini tangu kale wanaogeuka kuwa Wayahudi na kuingizwa ndani ya kundi lao, hadhi yao ni sawa na wale ambao wamezaliwa ndani ya kabila hilo.
Watu
Wayahudi wanapatikana hivi kwenye mabara ya Dunia (mnamo 2018):[1]
Mnamo mwaka2018 walikuwepo Wayahudi milioni 14.6 duniani. Hii inalingana na asilimia 0.19 ya watu wote duniani. Walio wengi wako katika nchi za Israel na Marekani.
Kutokana na harakati za kuhama, uenezi wa Wayahudi wakati wa karne ya 20 ulikuwa na mabadiliko mengi. Mnamo mwaka 1990Umoja wa Kisovyeti ulikuwa bado na idadi kubwa ya Wayahudi. Baada ya mwisho wa umoja huo wengi waliondoka kwenda hasa Israeli na Marekani na kwa idadi ndogo zaidi Ujerumani pia.
Takwimu ya mwaka 2018 nchi kwa nchi ni kama ifuatavyo.[1]
Historia yao ilianza katika sehemu zinazoitwa leo Israel na Palestina. Huko waliunda mnamo mwaka 1000 KKdola lao lililokwisha katika vita mbalimbali dhidi ya milki kubwa kama Ashuru na Babeli.
Wenyewe wanamkumbuka babu yao Abrahamu aliyeondoka Mesopotamia kwenda Kanaani walipojulikana kama Waebrania. Yakobo mjukuu wa Abrahamu aliitwa pia kwa jina Israeli na ndiyo asili ya kuita ukoo wote uliofuata "Wana wa Israeli“. Katika kumbukumbu yao, kizazi kilichofuata kilihamia Misri walipokaa kwa vizazi kadhaa na kuwa wengi. Kumbukumbu katika Kitabu cha Kutoka inasimulia jinsi gani Mfalme Farao wa Misri aliwalazimisha Waebrania kufanya kazi za watumwa na jinsi walivyoongozwa na Musa kutoka utumwa wa Misri wakijipanga kwa koo 12 au makabila 12 kufuatana na wana 12 wa Yakobo - Israeli.
Musa aliwaongoza Wanaisraeli kutoka Misri hadi jangwani. Huko waliunganishwa kama taifa moja wakipokea agano la Mungu aliyejifunua kwao kama YHWH kwenye mlima Sinai. Matukio hayo hukadiriwa mara nyingi yalitokea mnamo miaka 1300 KK au 1200 KK. Baada ya muda wa kutangatanga jangwani waliingia hatimaye katika nchi ya Kanaani na kupata nafasi yao kati ya makabila mengine walioishi huko.
Ufalme katika Kanaani - Palestina
Mnamo mwaka 1000 KK, makabila ya Wanaisraeli walimchagua mfalme wa kwanza Sauli na hapo waliishi katika utaratibu wa dola. Daudi na Sulemani ndio waliokuwa wafalme wakuu wakajenga mji wa kifalme wa Yerusalemu. Sulemani anakumbukwa kuwa alijenga hekalu ambapo makuhani waliendesha ibada na kutoa sadaka kwa Mungu wa Israeli.
Baada ya kifo cha Sulemani, Wanaisraeli waligawanyika katika falme mbili za Yuda huko kusini na Israeli huko kaskazini. Falme za Wanaisraeli walijikuta kati ya milki kubwa za siku zile zilizokuwa Misri kwa upande mmoja na milki za Mesopotamia ambako Wababeli, Waashuru na baadaye Waajemi walifuatana. Hatimaye Waashuru waliteka Ufalme wa Israeli mnamo mwaka 722 KK na kuhamisha wenyeji wengi hadi nchi za mbali. Yuda iliendelea hadi mwaka 586 KK wakati Wababeli waliharibu Yerusalemu pamoja na hekalu la Sulemani. Watu elfu nyingi hasa matabaka ya juu walihamishwa hadi Babeli.
Uhamisho wa kwanza
Tangu kuharibika kwa Yerusalemu mwaka 586 KK, idadi kubwa kiasi ya wenyeji waliishi nje ya Palestina wakilazimishwa kukaa Mesopotamia; wengine walikimbia Misri kwa usalama wao. Wakati vita ziliporudia kutokea katika karne zilizofuata, wenyeji wengine wa nchi walijiunga na ndugu zao waliowahi kuondoka.
Huko ugenini walianza kuitwa Wayahudi, yaani watu kutoka Yuda. Wakijifunza lugha mpya na tamaduni mpya walikazia pia urithi wa mapokeo yao ya kidini na kumbukumbu ya historia yao katika mazingira ambako wote waliabudu miungu mingi. Hasa huko Babeli, ambako familia za makuhani walipopelekwa, walikusanya mapokeo yote na kuyaunganisha kimaandishi. Sehemu nyingi za maandiko ya Biblia yalianza kupata huko umbo tunalojua hadi leo, ilhali kazi ya kukusanya na kupanga maandiko iliendelea baadaye. Wataalamu huamini kwamba hapa ugenini walianza pia desturi ya kukutana kwenye siku ya Sabato na kusoma maandiko matakatifu. Hapo ndipo chanzo cha Wayahudi kuwa „watu wa kitabu“ na cha mkazo wa pekee wa kusoma unaopatikana kati yao hadi leo. Kusoma maandiko kwao hakuwa kazi ya wataalamu pekee lakini iliendelea kuwa wajibu wa kila Myahudi.[6]
Kurudi Yerusalemu na Hekalu la Pili
Mwaka 538 KK Babeli ilishindwa na Milki ya Uajemi (leo: Iran) na Mfalme Koreshi aliwaruhusu Wayahudi kurudi Palestina na kujenga upya hekalu la Yerusalemu. Tunajua kwamba wako waliobaki na kuwa chanzo cha jumuiya ya Kiyahudi katika Mesopotamia na Babeli.
Wayahudi waliweza kujitawala ndani ya milki ya Uajemi kufuatana na sheria zao, wakiongozwa sasa na makuhani na wataalamu wa kidini. Hali hiyo iliendelea pia baada ya Aleksander Mashuhuri kushinda Uajemi. Palestina ilikuwa sasa jimbo la milki ya Kigiriki katika Syria. Katika kipindi hicho walianzisha sinagogi yaani nyumba ya mikutano hasa ya kidini ambapo maandiko yalisomwa.
Mwaka 166 KK Mfalme Mgiriki Antioko Epifane alijaribu kupiga marufuku sehemu za ibada za Wayahudi. Hapo Wamakabayo, jamii ya makuhani, waliongoza watu katika uasi wakafaulu kuanzisha dola la Kiyahudi katika Palestina.
Mnamo mwaka wa 140 hadi mwaka wa 37 KK walikuwa tena na wafalme wao. Baadaye walikuwa jimbo la Dola la Roma lakini walijaribu kuwafukuza Waroma mara mbili. Ilishindikana, hivyo hekalu la pili liliharibiwa mwaka 70BK, na Wayahudi wengi walipelekwa ugenini kama wafungwa na watumwa.
Uhamisho wa kudumu
Idadi ya Wayahudi walioondoka katika nchi yao iliongezeka kutokana na vita hizo, ambako pia wengi walipelekwa mbali kama watumwa. Jumuiya za Kiyahudi nje ya Palestina ziliongezeka na jumuiya mpya zilianza katika miji hadi Afrika Kaskazini na sehemu za Ulaya zilizokuwa pia chini ya utawala wa Kirumi. Chini ya Warumi, Wayahudi walitambuliwa kama jumuiya mojawapo yenye kanuni za pekee. Waliruhusiwa kukaa mbali na ibada za miungu mingi iliyokuwa dini rasmi ya Rumi. Katika mazigira mapya, Wayahudi wengi walitumia lugha ya Kigiriki. Wengine hawakuelewa tena Kiebrania, lugha ya mababu. Hata maandiko matakatifu yalitafsiriwa kwa lugha ya Kigiriki.
Tangu siku zile asilimia kubwa ya Wayahudi walikaa nje ya nchi ya mababu wakitawanyika sehemu zote za Dola la Roma na pia katika Milki ya Uajemi. Nchi za kigeni ndizo zimekuwa kama nyumbani kwa Wayahudi wengi wa Dunia.
Wayahudi chini ya Ukristo na Uislamu
Kuanzia mwaka 400 hivi, wakati Ukristo ulipokuwa dini rasmi ya Dola la Roma, ubaguzi wa kidini dhidi ya Wayahudi ulianza kwa viwango tofauti kwa karne nyingi. Wayahudi walikuwa dini pekee iliyovumiliwa nje ya Kanisa katika nchi za Wakristo, lakini viongozi wengine wa Ukristo walisikitikia kuwepo kwao. Katika nchi za Waislamu hali yao iliweza kuwa afadhali, kwa sababu huko walibaguliwa pia, lakini walikuwa dini mojawapo tu (pamoja na madhehebu ya Ukristo) waliovumiliwa chini ya Uislamu. Katika nchi za Waislamu Wayahudi waliona maendeleo kwa sababu waliweza kufanya kazi nyingi na kumiliki ardhi.
Hata hivyo, jumuiya za Wayahudi ziliweza kustawi katika nchi nyingi za Ulaya hadi mnamo mwaka 1000 hivi, hasa wakifanya biashara ya kimataifa lakini pia kama mafundi waliotafutwa. Wafayabiashara Wayahudi walikuwa muhimu kwa biashara kati ya maeneo ya Wakristo na Waislamu kwa sababu walikuwa na ndugu kila upande. Hali hiyo ilivunjwa tena na tena na vipindi vifupi vya mateso au mashambulizi kwa sababu mara kadhaa watawala au maaskofu hawakuwa tayari kuwavumilia.
Wayahudi wa Ulaya waliona mateso mara ya kwanza wakati wa Vita za Misalaba (1095 - 1291) kwa sababu watu wengi waliojitolea kwenda Yerusalemu hawakuelewa tofauti baina ya Wayahudi na Waislamu waliokuwa maadui katika vita hizo.
Mateso yaliendelea katika karne zilizofuata wakati wa milipuko ya tauni katika Ulaya iliyoua theluthi hadi nusu ya watu wote wa eneo fulani; jamii yote ilishikwa na hofu na mara kwa mara Wayahudi walituhumiwa kusababisha vifo kwa kutia sumu katika visima kwa sababu watu hawakuelewa hali ya ugonjwa wa kuambukizwa; mahali pengi Wayahudi waliuawa au walilazimshwa kupokea ubatizo.
Kukosa haki nyingi
Uwezo wa kiuchumi wa jumuyia za Kiyahudi katika Ulaya ulipungua sana, na wengi walibaki tu na nafasi ya biashara ya rejareja kwa sababu hawakupokewa katika jamii za mafundi na wafanyabiashara ya bidhaa fulani, pamoja na kutoruhusiwa kumiliki mashamba kwa sababu ya kutokuwa Wakristo.
Maisha ya Wayahudi yalikuwa magumu kwa sababu hawakuruhusiwa kuishi walipotaka, isipokuwa katika mitaa ya pekee ya miji iliyowaruhusu; mitaa hiyo iliyoitwa "ghetto" mara nyingi ilikuwa imejaa watu wengi mno. Sehemu ndogo ya Wayahudi waliruhusiwa kuishi nje ya miji katika maeneo ya makabaila waliowaruhusu.
Kazi zilizoweza kutekelezwa na Wayahudi katika nchi nyingi zilikuwa biashara ya rejareja, biashara ya mifugo na mazao na kukopesha pesa; ilhali Kanisa Katoliki lilipiga marufuku kukopesha kwa riba, watu waliomba Wayahudi kuwasaidia kwa kukopa. Kwa njia hiyo Wayahudi wachache walitajirika lakini walikuwa pia hatarini kwa sababu hawakulindwa kama raia; hivyo ilitokea tena na tena kwamba wakubwa walishtaki Myahudi aliyeshika madeni yao kwa makosa ya kidini au uwongo mwingine ili wasirudishe deni.
Ulaya ya Mashariki na Marekani
Hata hivyo kwa karne kadhaa hali yao ilikuwa afadhali katika ufalme wa Poland. Hivyo Wayahudi kutoka sehemu nyingi za Ulaya walihamia Poland (nchi za leo za Poland, Belarus na Ukraine). Tangu kugawiwa kwa Poland sehemu za hao Wayahudi wengi zilikuwa chini ya Urusi ambako ubaguzi dhidi yao uliongezeka.
Wakati wa karne ya 19serikali ya Urusi iliongeza sheria kali dhidi ya Wayahudi; pamoja na mashambulizi dhidi ya jumuiya zao Wayahudi wengi kutoka maeneo ya Milki ya Urusi walianza kuhamia Marekani. Pia Wayahudi kutoka nchi nyingine za Ulaya walioona ubaguzi mkali waliondoka na kuhamia Marekani.
Hivyo kwenye mwanzo wa karne ya 20 idadi kubwa ya Wayahudi walikuwa wakiishi katika Ulaya ya Mashariki na Marekani.
Mapinduzi ya Ufaransa na uhuru wa Wayahudi
Baada ya mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789 wananchi wote, wakiwa pamoja na Wayahudi, walipewa uraia. Hali hiyo, iliyoenea polepole katika nchi kadhaa za Ulaya ya Magharibi na Ulaya ya Kati, iliwaruhusu Wayahudi kuondoka katika ghetto, kufanya kazi zilizokataliwa awali na kusoma kwenye vyuo vikuu. Mwanzoni hawakukubaliwa katika vyeo vya juu vya utumishiserikalini. Katika karne ya 19 Wayahudi wengi walichukua nafasi hiyo wakasoma na kuingia katika fani za sheria, tiba, uandishi wa habari na nyinginezo. Kipindi hicho ndicho chanzo cha kutokea kwa wataalamu Wayahudi katika fani nyingi, waliofaulu kupata asilimia 20 za Tuzo za Nobel, hata kama Wayahudi hawafikii hata asilimia 1 ya watu wote duniani[7].
Kupanda kwa hadhi ya Wayahudi ambao hawakuonekana awali, kulisababisha kijicho. Wayahudi wengi walipokea ubatizo wakati ule ili waweze kutumia nafasi zote katika jamii. Kati ya Wayahudi wa Ulaya ya Kati na ya Magharibi lilitokea mwelekeo mpya wa matengenezo ambako sharika zao zilitafuta njia za ibada zilizolingana na nyakati za kisasa, ilhali sharika nyingine ziliendelea na mfumo wa zamani.
Ubaguzi mpya wa kimbari na maangamizi makuu dhidi ya Wayahudi wa Ulaya
Mafundisho mapya ya kibiolojia yalisababisha aina mpya ya ubaguzi wa kimbari dhidi ya Wayahudi; katika itikadi hiyo Wayahudi walichukiwa, si kwa sababu ya dini yao, bali kwa sababu ya asili yao ya nje ya Ulaya, katika Asia. Itikadi hiyo (kwa Kiingereza: antisemitism) ilisambaa katika sehemu za raia Wakristo na kuwa msingi kwa itikadi ya Adolf Hitler ya karne ya 20 iliyoleta maangamizi ya Wayahudi wa Ulaya wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Baada ya kushika serikali kwenye mwaka 1933, serikali ya Hitler ilifuta haki za kiraia za Wayahudi Wajerumani na kupora mali yao.
Katika Vita Kuu ya Pili ya Duniajeshi la Ujerumani lilivamia maeneo makubwa katika nchi jirani upande wa Mashariki ambako Wayahudi wengi waliishi. Mashambulio dhidi ya Urusi kwenye mwaka 1941 yaliandaliwa pamoja na vikosi maalum vilivyoteuliwa kwa shabaha ya kuua Wayahudi. Malakhi kadhaa walikusanywa na kuuawa kwa kupigwa risasi. Baada ya kuona uchovu upande wa askari wauaji, kambi za mauti zilianzishwa ambako watu waliuawa kwa gesi ya sumu. Katika kambi mashuhuri ya Auschwitz peke yake watu milioni 1 waliuawa. Wayahudi walikusanywa kote Ulaya wakapelekwa kwa reli kutoka nchi kama Ufaransa, Uholanzi, Ugiriki hadi kambi hizo. Vijana wenye nguvu walitengwa kwa sababu wakati wa vita Ujerumani ilikuwa na uhaba wa wafanyakazi wa viwandani ambako Wayahudi na wafungwa wengine walilazimishwa kufanya kazi bila malipo. Wengine waliuawa mara moja.
Madhulumu chini ya Ujerumani iliyoongozwa na Adolf Hitler yalisababisha vifo vya Wayahudi milioni 6 hivi; jumuiya za Kiyahudi katika nchi nyingi zilipotea kabisa, hasa katika Ulaya ya Kati na Ulaya Mashariki, isipokuwa Urusi yenyewe katika sehemu zake zisizovamiwa na Ujerumani.
Kuanzishwa kwa Dola la Israeli
Tokeo moja la kipindi hicho lilikuwa kuanzishwa kwa Dola la Israel mnamo 1948 baada ya Vita Kuu ya Pili. Wayahudi ambao walibaki katika kambi za mauti walioona kwamba familia zao haziko tena wala jumuiya zao za awali haziko tena walitafuta mahali papya pa kuishi wakajiunga na harakati ya kuhamia Palestina katika nchi ambako mababu wao waliwahi kuondoka miaka 2000 iliyopita. Harakati hiyo ya Uzayuni ilianza tangu mwanzo wa karne ya 20 lakini kabla ya mateso chini ya Hitler idadi ya Wayahudi waliowahi kuhamia Israel ilikuwa ndogo. Uhamiaji huo ulisababisha fitina kali na wenyeji Waarabu wa Palestina na vita ya uhuru wa Israel wa 1948-1949.
Vita hiyo ilisababisha pia mashambulizi dhidi ya Wayahudi walioishi katika nchi za Waarabu; tangu 1949 hadi 1980 Wayahudi 850,000 walifukuzwa, walikimbia au kuhama kwa njia nyingine hadi kufika Israeli[8] au Marekani, kwa asilimia ndogo pia Ulaya.
Israel inaendelea kama nchi ambako Wayahudi ni wengi wakiishi pamoja na asilimia 20 za raia Waarabu. Ugomvi na majirani haujapata usuluhisho bado ukasababisha vita nyingine na leo Dola la Israeli linasimamia Palestina yote ilhali Waarabu Wapalestina wako chini ya usimamizi wa kijeshi wa Israeli ilhali sehemu za Palestina zina pia serikali ya Kipalestina yenye madaraka machache.
Wayahudi ni wachache katika kila nchi wanamoishi, isipokuwa katika taifa la kisasa la Israeli.
↑Arnold Dashefsky, Sergio Della Pergola, Ira Sheskin (Hrsg.): World Jewish Population. 2018 (PDF) (Report). Berman Jewish DataBank. Abgerufen am 22. Juni 2019.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Wayahudi kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Strategi Solo vs Squad di Free Fire: Cara Menang Mudah!