Vita ni mapambano baina ya nchi, mataifa au angalau vikundi vikubwa vya watu yanayoendeshwa kwa nguvu ya silaha.
Katika vita kuna pande mbili au zaidi. Husababisha mateso, vifo na kuharibika kwa mali ya watu pamoja na mazingiraasilia.
Asili ya vita ilikuwa mapambano kwa silaha kati ya makabila au vijiji mbalimbali. Baada ya kutokea kwa madola ilikuwa zaidi serikali au watawala wa madola walioamua juu ya vita.
Aina za vita
Kuna aina tofauti za vita:
vita kati ya nchi mbili au zaidi kwa niaba ya serikali zao
vita ya uhuru ambako watu wa eneo fulani wanapambania dola ya pekee, kwa mfano
vita ya wenyeji wa koloni au nchi lindwa dhidi ya serikali ya kikoloni au nchi inayotawala
vita ya watu wa sehemu moja ya nchi dhidi ya serikali ya nchi nzima
Watekelezaji wa vita
Watekelezaji wa vita huitwa askari au wanajeshi. Historia imejua vipindi ambapo wanaume wote wa nchi fulani walitakiwa kushika silaha na kushiriki katika mapigano. Palikuwa pia na vipindi na utamaduni ambapo wapiganaji walikuwa watu wa pekee wenye jukumu hilo ama kwa sababu walipaswa kuwa askari kufuatana na sheria za nchi au kwa sababu walikodiwa kwa kazi hii.
Wanajeshi rasmi huwa chini ya kanuni za vita lakini sehemu kubwa na vita inashirikisha watu wasiofuata kanuni hizo kama wanamgambo hasa katika vita za wenyewe kwa wenyewe.
Silaha
Wanadamu wametumia akili nyingi kuboresha vifaa vya vita, yaani silaha, na mbinu za vita. Maendeleo ya silaha yamesababisha kupungua kwa idadi ya askari wanaopigana moja kwa moja lakini uharibifu wa silaha umeongezeka.
Silaha za kale zilitegemea nguvu ya mkono wa mtu zikifikia umbali mdogo. Silaha zimebadilika kulenga mahali ambapo ni mbali zaidi na zaidi. Silaha kali za kisasa zina uwezo wa kuharibu nchi yote; jumla ya silaha za nyuklia inatosha kuua uhai wote duniani.
Jitihada za kuepa au kupunguza athari za vita
Kutokana na uharibifu mkubwa unaosababishwa na vita palikuwa tena na tena na makubaliano juu ya kanuni za vita. Kanuni hizo hulenga kupunguza hasara inayosababishwa na mapigano. Lakini historia imejaa pia mifano ambapo kanuni hizo zilivunjwa au kupuuzwa.