Biashara hiyo ikabadilisha uso wa mji wa Zanzibar wa karne ya 19 uliowahi kuwa kijiji kikubwa tu cha vibanda kando ya boma lililojengwa na Omani kama kizuizi dhidi ya Wareno.
Baada ya azimio la mwaka 1832 la kuhamisha mji mkuu wa Omani kwenda Unguja, idadi ya wakazi wa mji ilikua haraka.
Waanglikana wa chama cha Misheni ya Vyuo Vikuu kwa Afrika ya Kati U.M.C.A. (Universities` Mission to Central Africa) ambacho kiliundwa ili kutekeleza wito kutoka David Livingstone kuhubiri Injili na kukomesha utumwa katika Afrika, waliingia Zanzibar mwaka 1864.
Baadaye wakajenga kanisa kuu mahali pa soko la watumwa lililofungwa, altari ikiwa imejengwa juu ya nafasi ya mti wa kuwafunga watumwa walioadhibiwa kwa viboko, na batizio kuwa mahali walipotupwa watoto watumwa ambao hawakuuzwa pamoja na mama zao.
Sultani wa pili wa Zanzibar yenyewe, Sayyid Barghash (1870-1888), alijitahidi kujenga uhusiano na nchi za nje. Alifunga soko la watumwa Zanzibar mjini kulingana na mapatano ya kimataifa, lakini akavumilia biashara ya watumwa kuendelea chinichini. Wakati wa Barghash majengo mengi ya Mji Mkongwe yakajengwa.
Barghash alikuwa na wanajeshi wa kudumu. Mwanzoni alitumia mamluki walioajiriwa kutoka Uarabuni na Uajemi, hasa Baluchistan, pamoja na watumwa[1]. Kuanzia mwaka 1877 alianzisha kikosi kipya cha askari mia kadhaa chini ya afisa Mwingereza Lloyd Mathews waliofundishwa kufuatana na utaratibu wa Kizungu; askari hao waliteuliwa chini ya Waafrika wa Unguja.[2]
Mwishowe mwa utawala wake aliona kupungukiwa kwa eneo lake kutokana na mashindano ya nchi za Ulaya ya kuenea katika Afrika baada ya mkutano wa Berlin wa 1885.
Mwaka 1885Karl Peters alifanya mikataba ya ulinzi na watawala wadogo waliokuwa chini ya Sultani barani Tanganyika. Upingamizi wa Sultani ulishindikana kwa sababu Wajerumani walituma manowari Unguja akapaswa kukubali maeneo mapya ya Wajerumani.
Kuenea kwa ukoloni
Mwaka 1886mkataba kati ya Uingereza na Ujerumani ulibana eneo la sultani barani katika kanda yenye upana wa maili kumi tu kati ya Rasi Delgado na Mogadishu. Barghash na mfuasi wake Khalifa bin Said waliamua kuuza maeneo hayo au kuyakodisha.
1887/1888 pwani ya Kenya ilikodishwa kwa Waingereza. Wakati wa uhuru wa Kenya sehemu hii ikaingizwa katika Jamhuri ya Kenya.
Pwani ya Tanganyika ikakodishwa kwa Wajerumani mwaka 1888 na hatimaye kuuzwa mwaka 1890.
Miji kwenye pwani ya Somalia ikakodishwa kwa Italia mwaka 1892 ikauzwa mwaka 1906, ila Mogadishu mwaka 1924.
Hali halisi usultani ukabaki na visiwa viwili vya Unguja na Pemba tu.
Waingereza walikuwa walisita kuhusu Zanzibar lakini baada ya jaribio la Karl Peters la kufanya mkataba na Sultani ili kuingiza visiwa hivyo katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, Uingereza uliamua kutafuta utawala wa visiwa.