Afrika Mashariki katika miaka 1800-1845 ilikuwa na mabadiliko makubwa kama ifuatavyo.
Jumuiya za Pwani na Bara kabla ya 1800
Jumuiya za pwani zilikuwa zimetengana, kila moja ikiwa huru kutoka kwa nyingine na kila moja ikiwa na watawala wake. Athari za jumla za Waarabu wa Oman zilikuwepo Mombasa, Zanzibar na Kilwa tu, na hata katika maeneo hayo Waarabu hao waligawana madaraka na wenyeji wa Kiswahili na wa Kishirazi.
Huko Mombasa, viongozi wa wenyeji – Waswahili - walishiriki katika uendeshaji wa siasa wa mji huo. Familia ya Mazrui toka Oman iliendelea kuwa huru kutoka kwa watawala wa Kioman wa Zanzibar kwa sababu ya ushirikiano wao wa karibu na masheikh wenyeji wa Kiswahili ambao walichangia nao utawala. Hata kwa kipindi fulani, baada ya utawala wa Wamazrui kupinduliwa, viongozi wa Kiswahili waliendelea kuwa mashuhuri katika uendeshaji wa mji.
Watawala wa kienyeji wa Zanzibar walianza kupoteza mamlaka yao kisiasa kadiri Waomani walivyozidi kuimarika katika funguvisiwa hili. Wakati huohuo, wenyeji wa Zanzibar walipokonywa ardhi na walowezi wa Kiomani ambao waliyanyemelea hasa maeneo yenye rutuba kaskazini na mashariki mwa kisiwa.
Pamoja na kuwepo kikosi cha kulinda ngome cha Waomani kwenye kisiwa cha Kilwa, Sultani mwenyeji alibakishiwa cheo chake na sehemu ya moja ya tano ya ushuru, na alikuwa na mamlaka yake kiutawala kwenye pwani ng’ambo ya Kilwa Kisiwani. Upotevu wa mamlaka yake haukusababishwa tu na kuwepo kwa Waomani, bali pia kudhoofika kiuchumi kwa Kilwa Kisiwani yenyewe, kulikosababishwa na kuinuka kwa mji pinzani wa Kilwa Kivinje huko bara, ambao ulifanikiwa kuelekeza biashara ya watumwa na meno ya ndovu kutoka kisiwani kwenda depo ya bara.
Ilipofika mwaka 1800, Malindi, mji mwingine miongoni mwa miji ya pwani, ulikuwa umefifia sana kutokana na familia yake ya kiutawala kuhamia Mombasa kwenye karne ya 16.
Kaskazini mwa Malindi vilikuwepo visiwa vya Lamu na Pate. Ilipofikia 1800, Pate ilikuwa imeshaporomoka kutoka kwenye nafasi ya umashuhuri wa kibiashara iliyokuwa nayo katika karne ya 17 na ya 18 kutokana na migogoro ya urithi na mapambano na kisiwa jirani cha Lamu. Ushindani kati ya visiwa hivyo viwili baadaye ulirahisisha kuingiliwa na kutawaliwa kwao na Zanzibar.
Barani, mkabala na visiwa vya Lamu na Pate, waliishi Wabajuni ambao walienea pia kwenye mlolongo wa visiwa vidogovidogo vya pwani ya Somalia.
Usultani wa Omani
Kuibuka na kukua kwa athari ya Oman katika Afrika Mashariki kulikuwa matokeo ya mambo mbalimbali, baadhi yake yakiwa ndani ya Usultani wa Omani, na baadhi kutoka nje. Hata hivyo, jambo muhimu zaidi bila shaka lilikuwa tamaa za kiuchumi na werevu wa Sultani Seyyid Said (1806-1856), ambaye alijichukilia awali ya yote kuwa mwanamfalme mfanyabiashara. Kwa kufuata sera ya kutofungamana na upande wowote kati ya Ufaransa na Uingereza wakati wa vita vya Napoleon, Said aliweza kupanua mahusiano ya safari za baharini na ya nje ya Oman hadi kufikia kiwango ambapo alikuwa tishio hasa kwa meli za Uingereza, na mataifa yote hayo mawili yalijitahidi kufanya urafiki naye. Hususani Waingeraza, ili kuilinda njia yao ya biashara ya kuelekea India, walimsaidia Said kujiimarisha Oman, na hatimaye wakaitwa Aden mwaka 1839.
Utengano wa ndani ya nchi yake ulimwezesha Seyyid Said kupanua uchumi wake pasi na vikwazo. Aliona kuwepo kwa mifarakano na udhaifu kwenye pwani ya Afrika Mashariki kuwa fursa nzuri kwa upanuzi wa kiuchumi na wa kisiasa. Aidha aliona haja ya kupambana na tamaa ya nchi za Ulaya kwa kukita mikakati yake mwenyewe.
Alianza kufanya mawasiliano na wenyeji na watawala kwa kushauriana na kufanya mikataba nao, na kujihusisha kwenye ushindani wa wao kwa wao.
Ulipokifia mwaka 1823, alikuwa amekwisha kufaulu kuwa na mashiko katika visiwa vya Pate na Lamu, na jumuiya chache za jirani. Wapinzani wake wakuu walikuwa ni Wamazrui – nasaba ya kifalme iliyotawala Mombasa, pia wakiwa na chimbuko la Oman – ambao waliishawishi Uingereza kuweka Mombasa chini ya ulinzi wao mwaka 1824.
Hatua hii iliharibu kwa kiasi fulani mahusiano kati ya Sultan Said na Uingereza. Hata hivyo ulinzi huo wa Waingereza haukudumu muda mrefu kwa sababu Waingereza walionyesha kumpendelea Said, na Wamazrui hawakuwa na raghba tena juu ya ulindwaji huo kwa vile uliwalazimisha kugawana ushuru wao na Waingereza ambao walikuwa wameshindwa kuwasaidia (Wamazrui) kurejesha maeneo yao yaliyotekwa.
Uhusiano wa kibiashara wa Pwani/Bara
Muda mfupi baada ya Said kupata udhibiti wa Mombasa aliamua kuhamisha makao makuu ya usultani wake kwenda Zanzibar, mji ambao ulikuwa ukikua kwa haraka kama kituo cha kibiashara chenye shughuli nyingi. Said alivutiwa sio tu na suhula za kimeli za Zanzibar, bali pia na rutuba ya kisiwa na uwezekano wake wa kuzalisha mazao ya kilimo. Aliamua kuhodhi biashara yote ya kisiwa na akaendelea kukifanya kuwa kituo kikuu cha uchumi katika pwani ya Afrika Mashariki.
Baadhi ya bidhaa za biashara zilizopatikana hapo ni meno ya ndovu, watumwa, karafuu, sandarasi, simbi na bidhaa za kutoka nje kama vile nguo za pamba, shanga, nyaya, mikufu, magobori, baruti, vyombo vya kauri, kioo (vyombo vya kioo), visu na mashoka.
Nafasi ya Zanzibar iliimarika pia kutokana na kutambulika kwake kupitia mikataba ya kibiashara na mataifa ya nje kama vile Marekani, Uingereza na Ufaransa.
Meno ya ndovu na watumwa ndizo bidhaa zilizokuwa na faida kubwa zaidi kwa usultani wa Oman kwa sababu ya mahitaji yake makubwa ndani na nje ya nchi. Wayao, kikundi cha bara, walikuwa na mtandao wa biashara ya masafa marefu waliotumia kuleta pwani meno ya ndovu na watumwa. Shughuli zao zilienea kuzunguka ziwa Nyasa, na bidhaa zao zilifika pwani ya Zanzibar kupitia Kilwa Kivinje. Kwa hakika kukua kwa umaarufu na ustawi wa Kilwa Kivinje kulitokana na kuongezeka kwa mashirikiano ya kibiashara kati ya watu wa pwani na bara katika karne ya 19.
Watumwa walipatikana kupitia mashambulizi na vita, ingawa si mapigano na mashambulizi yote yaliyotokea yalisababishwa na haja ya kuteka watumwa. Zaidi ya hayo, watu waliotiwa utumwani mara nyingi walitoka katika vikundi vya bara ambavyo vilikuwa vikifanya biashara ya watumwa kama vile Wayao, Wabisa, Wamakua na Wangindu.
Walikuwepo wafanyabiashara ya masafa marefu wengine kwenye eneo la kaskazini mwa ziwa Nyasa; waliokuwa mashuhuri zaidi ni Wanyamwezi, Wakamba na Wamijikenda. Hao walianzisha mahusiano na pwani kwa mara ya kwanza kunako takribani mwaka 1800, na baada ya muda mfupi wakaimarisha mitandao ya kibiashara kati ya eneo hilo la bara na pwani.
Kadiri bei za watumwa na meno ya ndovu zilivyozidi kupanda, baadhi ya wafanyabiashara wasio Waafrika walianza kuingia bara. Msafara wa kwanza ulioongozwa na wasio Waafrika kuelekea bara ulifika Unyamwezini mwaka 1824 na ilipofikia 1845, wafanyabiashara wengi wa pwani, hasa Waarabu, walikuwa wamekwisha penya ndani ya bara hadi kufikia Buganda.
Athari za kijamii na kiuchumi za biashara iliyokuwa inapanuka
Upanuzi wa biashara katika pwani na bara ya Afrika Mashariki ulikuwa na athari zake muhimu. Kwa mfano, upanuzi wa Wakamba nje ya makazi yao ya asili hadi kufikia kwenye maeneo ambayo hayakuwa na rutuba ya kutosha uliwafanya waanze uwindaji, ufugaji na biashara za kubadilishana mali kama njia ya kujikimu. Walifanya biashara na majirani zao kama vile Wakikuyu, Waembu na Wamasai, na hatimaye wakapanua mtandao wao wa biashara hadi pwani. Waliandaa misafara yao kwenda pwani na waliongoza katika biashara ya masafa marefu kwenye maeneo ya kaskazini ya bara ya Afrika Mashariki hadi miaka ya 1850, nafasi yao ilipochukuliwa na Waarabu na Waswahili.
Kutokana na mahusiano hayo ya kibiashara kati ya pwani na bara, mfumo wa kuishi katika makazi yenye ngome ya Wamiji kenda yaliyoitwa kaya ulianza kudhoofika. Watu walianza kuziacha kaya ili kwenda kufanya biashara. Mtawanyiko huu ulififisha umoja na mshikamano wa kaya, ukamomonyoa mamlaka ya wazee na kuua mfumo wa uongozi wa marika.
Kadhalika, waliibuka matajiri waliokuwa na wafuasi na waliojijengea umaarufu. Miongoni mwa matajiri hao ni Ngonyo wa Kigiriama, Mwakikonge wa Kidigo na Kivui wa Kikamba.
Athari nyingine ilikuwa desturi ya kuoa wake wa kigeni. Kuoana huku miongoni mwa vikundi tofautitofauti kulipelekea kuanzishwa kwa undugu miongoni mwa jamii zilizohusika. Maingiliano ya kiutamaduni kati ya Wabantu na Waarabu, na kati ya Wabantu na Waswahili yalitokana na kukua kwa matumizi ya watumwa wa nyumbani (wa kazi za ndani) kwenye mashamba na kuenea kwa usuria.
Katika usultani wa Oman desturi ya kuoa wake wa kigeni ilikuwa imeenea sana, hasa miongoni mwa tabaka la watawala. Maingiliano ya kiutamaduni kati ya Waarabu na wenyeji wao huko pwani yalikuwa makubwa kiasi kwamba kulikuwepo na tofauti bayana za kiutamaduni kati ya Waarabu wa Oman walioishi nyumbani (Uarabuni) na wenzao “walio-Afrikishwa” na kuishi katika miji ya Kiswahili.
Hali kadhalika kulikuwepo na mabadiliko kadhaa huko bara yaliyotokana na kushiriki kwa watu katika biashara ya pwani. Baadhi ya watawala wa bara walijenga upya miji yao mikubwa kwa mtindo wa pwani, wakipamba vitala vyao na bidhaa za pwani na hata kukuza hamu ya vyakula vya pwani.
Lugha ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano mapana ya tabaka la wafanyabiashara pia ilienea sana huko bara. Mwanzo ilikuwa ikitumika kama lugha ya kibiashara, lakini muda ulivyozidi kusogea ndivyo na matumizi ya lugha yalivyoongezeka miongoni mwa wakazi wa bara.
Miongoni mwa matukio muhimu ya kijamii na kisiasa yaliyotokea miongoni mwa watu wa eneo la Maziwa Makubwa ni kuibuka kwa jumuiya kamili za kisiasa zenye utambulisho maalum kama ile ya Buganda. Buganda ilistawi kama dola unganifu yenye asasi sanifu za kisiasa. Lakini vikundi vya mashariki mwa ziwa Viktoria, isipokuwa ufalme wa Wawanga, havikuanzisha dola zozote unganifu.
Hata hivyo, si vikundi vyote vya bara viliathiriwa na utamaduni wa pwani. Wakikuyu, kwa mfano, hawakuonyesha raghba yoyote katika biashara ya pwani, hata wakati wa misafara ya Waarabu na Waswahili ilipoingia katika ardhi yao. Wamasai waliwazuia wafanyabiashara wa Kiarabu na Kiswahili kuingia katika ardhi yao.
Biashara ya kimataifa ya Oman
Seyyid Said alitekeleza sera ya uchumi ya kuhimiza biashara na makazi ya Wahindi katika Zanzibar.
Waasia hao walikuwa na busara nyingi katika kufanya biashara na walishika nafasi zilizo muhimu kabisa kama mawakala wa ushuru, walanguzi, mabepari na wakopeshaji fedha na wafanyabiashara ya jumla ya nchini Zanzibar. Ingawa kuwepo kwao na shughuli zao huko Zanzibar hazikuwapatia sauti yoyote katika siasa na uendeshaji wa shughuli za kiserikali, nafasi yao ya kiuchumi iliimarika sana. Baadhi yao walitajirika sana, kiasi kwamba hata baadhi ya Masultani wa Zanzibar waliwakopa fedha.
Said pia alianzisha kilimo cha karafuu kisiwani Zanzibar. Alitumia nguvukazi ya watumwa kuendeleza tasnia ya karafuu akawa mwuzaji mkuu nchi za nje wa zao hili lililofika hadi Bombay nchini India. Kwa hakika, ilipofika 1843, India ilikwisha kuwa mnunuzi mkuu wa karafuu za Zanzibar.
Kutokana na kuongezeka kwa umaarufu wa karafuu, Waarabu wa Kiomani kadhaa katika visiwa vya Zanzibar na Pemba walianza kulima karafuu katika mashamba makubwa. Jambo hili lilikuwa na matokeo mengi:
- lilivunja ukiritimba wa Said katika biashara ya karafuu.
- lilipelekea kwenye kufanya karafuu iwe tasnia ya kitaifa miongoni mwa Waarabu wa Oman.
- liliongeza mahitaji ya nguvukazi ya watumwa, pia liliongeza biashara ya watumwa ya Afrika Mashariki.
- lilifanya mazao mengine yapuuzwe kama vile nazi na mpunga.
- ilileta matatizo ya ardhi kisiwani Zanzibar. Matatizo hayo ya ardhi hasa yaliharibu kwa kiasi fulani mahusiano kati ya Waarabu wa Oman na wakazi wa asili wa Zanzibar walioporwa ardhi yao na Waarabu.
Hata hivyo sera za kibiashara na za kiuchumi za Said sio tu ziliifanya Zanzibar kuwa kituo kikuu cha kibiashara kwenye pwani ya Afrika Mashariki, bali pia polepole ziliuingiza uchumi wa Afrika Mashariki kwenye mfumo wa kibepari wa (nchi za) Magharibi.
Taathira hasi ya hali hii ni kwamba wafanyabiashara kutoka Ulaya, Marekani na Asia walitajirika kwa kuwafukarisha wenyeji wa Afrika Mashariki, na hivyo kusababisha kudumaa kwa maendeleo yao. Rasilimali (watu na nyenzo) za Afrika Mashariki zilinyonywa kupitia ubadilishanaji usio na usawa uliokuwa ukifanywa kati ya wafanyabiashara wa kigeni na wenyeji.
Hitimisho
Kulikuwepo pia na ukuaji wa biashara ya masafa marefu ulioanzishwa na vikundi vya Waafrika huko bara. Baadaye, wafanyabiashara wa Kiarabu na wa Kiswahili walikwenda hadi bara kutafuta bidhaa zaidi. Biashara ya masafa marefu ilikuwa ikipanuka na kuwa na athari zake za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni kwa vikundi vingi vya bara. Athari hizo zilijumuisha uenezi wa Uislamu na lugha ya Kiswahili.
Lakini baadhi ya matukio muhimu kama vile uvamizi wa Wanguni yalitokea bara pasi na kuhusiana na biashara ya masafa marefu.
Maendeleo ya ukuaji wa athari za kibiashara za Zanzibar yalipelekea kwenye ubadilishanaji (wa bidhaa) usio na usawa kati ya Afrika Mashariki na (nchi za) Magharibi. Aidha yaliuingiza uchumi wa Afrika Mashariki kwenye mfumo wa kipebari na hivyo kusababisha kudumaa kwa maendeleo ya eneo hili.
Angalia pia
Marejeo
- Bennett, N.R. (1981) A History of the Arab State of Zanzibar (London: Methuen)
- Berger, I. (1981) Religion and Resistance in East African Kingdoms in the Precolonial Period (Tervuren: Musée royal de l'Afrique centrale)
- Sutton, J. E. G. (1973). Early trade in Eastern Africa (Nairobi : East African Publishing House)
Viungo vya Nje