Lamu lina umbo la kanda ndefu mwambaoni. Mji wa kale umegawiwa katika mitaaarobaini lakini kuna hasa sehemu mbili: Mkomani upande wa kaskazini penye nyumba kubwa ya mawe na Langoni upande wa kusini ambako wakazi wapya walijenga nyumba za udongo.
Jengo kubwa la mji ni boma lililokaa zamani moja kwa moja ufukoni.
Mwambao wa leo umepatikana tu tangu karne ya 19. Mwambao wa kale unaonekana kwa barabara ya Harambee (au: Usita wa Mui). Wakati wa kujenga Boma ufuko wa kale ulikuwa na maji yenye kina kifupi, hivyo ikaamuliwa kujaza sehemu hizo na kupanua eneo la mji kuingia ufukoni. Watu wenye uwezo walijenga nyumba zao kubwa na mstari wa ufuko ukaimarishwa kwa ukuta.
Wareno walifika Lamu mwaka1506. Watawala wa Lamu walipaswa kupatana nao ingawa kuna taarifa za majaribio kadhaa za kuasi. Lamu haikuwa kati ya miji kama Malindi iliyoshikamana na Wareno kwa hiari. Mji ulitumia nafasi mbalimbali kuasi dhidi ya Wareno ukaabishiwa vikali kila safari hadi mwishowe Waarabu wa Omani waliwaondoa Wareno mnamo 1696 kabla ya kuteka kituo chao cha mwisho huko Mombasa mwaka 1698.
Karne za dhahabu
Kuja kwa Wareno kulikuwa kumevuruga biashara ya Bahari Hindi pamoja na heri ya miji mingi ya Waswahili. Kuondoka kwao kulimaanisha ya kwamba nafasi hizo zikapatikana tena. Omani ilikuwa na utawala wa pwani ya Afrika ya Mashariki lakini kwa mbali tu na utawala wake haukuwa mzogo sana. Lamu ilianza kustawi kushinda miaka ya nyuma. Majengo mazuri yanayopamba mji wa kale yalijengwa wakati wa karne ya 18 na hasa ya 19.
Hadi mwisho wa karne Lamu ilikuwa mji wa kwanza katika funguvisiwa. Umuhimu wa biashara ya watumwa waliouzwa Zanzibar na Uarabuni ikaongezeka na kazi ya watumwa iliwezesha mabwana kulima mashamba makubwa wakiuza mazao nje.
Kukwama na kurudi nyuma
Sehemu ya pili ya karne ya 19 iliona mabadiliko tena. Usultani wa Zanzibar ulikuwa umerithi ubwana wa pwani kutoka Omani lakini uliweza kukazia utawala wake kwa sababu haukuwa mbali mno.
Katika miaka tangu 1880 nchi za Ulaya zilianza kujenga ukoloni wao. Wajerumani walianzisha koloni lao katika Witu wakajenga ofisi ya Posta ya Kijerumani kwenye mji wa Lamu kwa sababu palikuwa na bandari iliyo karibu zaidi. Lakini kuja kwa Wazungu na meli zao kubwa kuliondoa pia sehemu ya biashara kutoka Lamu. Meli kubwa zilipendelea bandari kubwa zaidi kama Mombasa au Malindi.
Mwisho wa utumwa
Pigo kubwa kwa Lamu ilikuwa kukatazwa kwa utumwa. Waingereza walikuwa wakilazimisha Zanzibar kukataza kwanza biashara ya watumwa na baadaye utumwa wenyewe. Mabwana wote wenye mashamba makubwa kwenye pwani ya Uswahilini walishindwa kuendelea na mashamba yao na kupata faida kwa sababu waliokuwa watumwa hawakutaka tena kuwahudumia kama watu huru.
Eneo lililosahauliwa katika Kenya huru
Lamu ikakwama na kurudi nyuma katika Kenya iliyoona mabadiliko ya haraka wakati wa ukoloni na baadaye wakati wa uhuru. Wilaya ya Lamu ilipaswa kubeba mzigo wa kusahauliwa kama maeneo mengine ya nchi nje ya nyanda za juu. Barabara ya lami haikupatikana wilaya ya Lamu hadi mwaka 2006.
Miaka ya mwisho utalii umeleta tena biashara mpya lakini mara nyingi ni watu wa nje ya Lamu wanaofaidika.
Utamaduni
Mifano bora ya usanifu wa Uswahilini inapatikana Lamu. Hivyo imepokewa na UNESCO katika orodha ya urithi wa dunia kwa sababu ni "mji wa Uswahilini uliohifadhiwa kushinda miji yote mingine".
Boma la Lamu lililojengwa na watu wa Pate leo hii ni makumbusho yanayotembelewa na wageni wengi.
Makumbusho madogo yanakumbusha kituo cha kwanza cha posta ya Kijerumani katika Afrika ya Mashariki; Lamu ilikuwa kituo cha posta kwa koloni la Kijerumani huko Witu.