Eneo la mji ni kati ya m 1600 kitovuni na m 1900 au zaidi juu ya UB kwenye mitelemko ya mlima Loleza.
Hali ya hewa haina joto kali kutokana na kimo. Wakati wa Juni-Julai halijoto wakati wa usiku inaweza kushuka chini hadi 0 °C, mlimani hata chini zaidi.
Mvua zinaanza mwezi Novemba hivyo ni wakati wa kupanda. Kwa kawaida mvua zinasimama tena Januari-Februari na kunyesha kwa wingi Machi-Aprili.
Kitovu kipya cha mji kinahamishwa kwenda kata ya Foresti iliyoko kando ya barabara kuu.
Historia
Jina la Mbeya limetokana na neno la Kisafwa "Ibheya" ambayo maana yake ni chumvi, kwani miaka mingi wafanyabiashara walikuwa wanafika mahali hapo kubadilishana mazao yao kwa chumvi.
Mlima mkubwa ulio karibu ulijulikana kwa jina la "Mbeya"[1] wakati wa ukoloni wa Kijerumani, na mji ulipokea baadaye jina kutokana na mlima huu.
Mji wa kisasa wa Mbeya ulianzishwa na wakoloniWaingereza mnamo mwaka 1927. Wakati ule dhahabu ilianza kupatikana mlimani karibu na Mbeya hadi Chunya.
Historia inavyoonekana katika jiografia ya Mbeya
Mji ulianzishwa katika sehemu zinazoitwa bado Uhindini, Uzunguni na Majengo. Mji ulipangwa kufuatana na kawaida ya miji wa kikoloni ya Afrika ya Mashariki kuwa na sehemu tatu:
Mahali pa makanisa ya kale panaonyesha ugawaji huu wa kihistoria:
Kanisa la Anglikana lililokuwa dhehebu rasmi la Uingereza lipo chini ya Uzunguni na karibu na ofisi za kiserikali (zinazoelekea siku hizi kuhamishwa kwenda Foresti) kama Mkuu wa Mkoa na mahakama. Kanisa hili ni jengo dogo kwa sababu lilipangwa kwa kundi dogo la maafisa na wafanyabiashara pamoja na wakulima Waingereza wa Mbeya.
Kanisa la mjini la Moravian, ambalo ni dhehebu la Kikristo asilia la Mbeya liko Majengo iliyokuwa sehemu kwa Waafrika. Kati ya Waingereza hawakuwepo Wamoravian.
Kanisa KuuKatoliki lilihudumia Wazungu wachache, hasa Waeire, kati ya wakoloni pamoja na Wahindi kutoka Goa na pia Waafrika: kwa hiyo iko kati ya Uzunguni na Uhindini karibu na Majengo.
Mji uliendelea kupanuka pande zote. Barabara kuu ya TANZAM inaunganisha sehemu za nje kati ya Uyole na Mbalizi.
Vilevile njia ya reli ya TAZARA hupita Mbeya kuelekea Zambia. Kuna ghala kubwa kwa ajili ya mizigo ya Malawi inayofikishwa kwa reli kutoka Dar es Salaam bandarini ikihamishwa kwa malori kwenda Malawi.
Mbeya imekuwa na uwanja wa ndege mdogo usiokuwa na huduma ya kawaida kwa muda mrefu. Lakini kuna mipango ya kujenga uwanja mpya huko Songwe zipatazo km 40 kufuata njia ya kwenda Zambia.
Tangu miaka ya 1990 kitovu cha mji kinahamishwa kutoka eneo la zamani kwenda karibu na barabara kuu ya Dar es Salaam – Zambia.
Wakazi
Mbeya ni mji wa nne kwa ukubwa nchini Tanzania. Idadi ya wakazi imehesabiwa kuwa 385,279 katika sensa ya mwaka 2012. Katika sensa ya mwaka 2022 walihesabiwa 541,603 [2]. Wengine 300,000 hivi wanaishi katika mazingira karibu na Mbeya mjini.
Uchumi wa Mbeya mjini umetegemea kilimo cha mazingira yake na biashara.
Viwanda mbalimbali vilianzishwa, lakini havikufaulu sana. Kuna viwanda kwa mfano Zana za kilimo, Highland Soap, Mbeya Textiles. Mbeya Ceramics iliporomoka kitambo.
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mbeya bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Mbeya (mji) kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.
Strategi Solo vs Squad di Free Fire: Cara Menang Mudah!