Katika umri mdogo wa miaka 22 Washington alijikuta kama mkuu wa wanamgambo katika vita vya Uingereza dhidi ya Wafaransa na Waindio vilivyopanuka baadaye kuwa Vita ya Miaka Saba. Akaongoza kikosi chake dhidi ya maadui akafaulu mara kadhaa.
Baadaye alishirikiana na jeshi rasmi la Uingereza katika mapigano ya Monongahela na kuongoza mabaki ya jeshi baada ya kifo cha jemadari Mwingereza. Mwaka 1755 akawa mkuu wa jeshi la koloni la Virginia. Lakini baada ya ushindi Waingereza walikataa kumpa cheo katika jeshi la mfalme, hivyo akajiuzulu akarudi kwenye shamba lake na kufuata siasa kwenye bunge la koloni.
Mwaka 1759 Washington akaoa mjane tajiri akawa kati ya matajiri wakuu kabisa wa Virginia.
Mapinduzi
Baada ya vita ya miaka saba uhusiano kati ya Uingereza na walowezi Waingereza katika makoloni yake 13 ya Amerika ya Kaskazini ukazorota. Tangu mwaka 1773 Waingereza walitumia sheria ya dharura na nguvu ya kijeshi mjiniBoston. Wawakilishi wa makoloni yote 13 wakakutana kama bunge la Amerika Bara na Washington alikuwa miongoni mwao.
Baada ya mapigano ya kwanza kati ya wanajeshi Waingereza na wanamgambo wa walowezi, bunge likaamua kuunda jeshi la pamoja la makoloni yote na Washington akateuliwa kuwa jemadari mkuu.
Baada ya uhuru wa Marekani George Washington akarudi kwake akalima tena lakini akachaguliwa pia kama mwakilishi wa Virginia katika bunge la katiba la Marekani mwaka 1787 akawa mwenyekiti wa mkutano huu uliokubali katiba ya Marekani.
Tarehe4 Februari1789 alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa Marekani akirudishwa mwaka 1789. Baada ya kipindi chake cha pili alikataa kusimama tena akaunda hivyo utaratibu wa kwamba rais anaweza kurudishwa mara moja tu, hawezi kuendelea zaidi.
Mwisho na heshima baada ya kifo
Mwaka 1797 akarudi tena kwake shambani aliposimamia kilimo kilichoendeshwa na watumwa 390. Tarehe 14 Desemba 1799 alikufa kwake nyumbani. Kabla ya kuaga dunia aliamuru katika usia wake ya kwamba watumwa wake wote wapewe uhuru baada ya kifo chake yeye mwenyewe na mke wake.