Njia ya kuunganisha Baltiki na Bahari ya Kaskazini ni milangobahari ya Kattegat na Skagerak. Mwanzoni wa Kattegat njia inapita kwenye visiwa vya Denmark na kuigawa katika njia tatu ndogo zinazoitwa Oresund, Belt Kubwa (Kidenmark: Storebælt) na Belt Ndogo (Kidenmark: Lillebælt).
Enzi ya Barafu
Kijiografia Baltiki ni mabaki ya Enzi ya Barafu iliyopita. Takriban miaka 12,000 iliyopita Ulaya yote ya Kaskazini ilifunikwa na ganda la barafu lenye unene wa mitamia kadhaa. Wakati wa kupungua kwa baridi barafu ilianza kuyeyuka na kusababisha kutokea kwa ziwa kubwa sana ambalo ni mwanzo wa Baltiki. Ziwa hili lilipata njia ya kujiunga na bahari na kiasi cha maji ya chumvi yaliingia ndani. Hivyo maji ya Baltiki ni mchanganyiko wa maji ya chumvi na maji matamu. Kiasi cha chumvi ndani ya maji yake ni kidogo kulingana na maji ya bahari ya kawaida.
Bahari yenye chumvi kidogo
Kiasi cha chumvi ni kikubwa zaidi kwenye kina kuliko kwenye maji ya juu. Wakati maji yenye chumvi kidogo inatoka kwenye Kattegat kuelekea Bahari ya Kaskazini kuna pia mwendo wa maji ya chumvi chini yake ya kuingia katika Baltiki. Maji ya chumvi ni mazito kuliko maji matamu, hivyo yanakaa kwenye vilindi vya bahari na kuwa na mwendo wa kuingia ilhali wakati huohuo maji ambayo ni matamu zaidi yanapita juu yake kutoka Baltiki.
Mito ya Baltiki
Mito mikubwa inaingia katika Baltiki na kusababisha mwendo wa maji ya kutoka katika Kattegat na kuingia Atlantiki. Baadhi ya mito hiyo ni: Oder, Vistula, Neman, Daugava na Neva.
Makala hii kuhusu maeneo ya Ulaya bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Bahari ya Baltiki kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.