Atlantiki ni bahari kubwa inayotenganisha Amerika upande wa magharibi na Afrika na Ulaya upande wa mashariki. Eneo lake ni kilometa za mraba 106,200,000 au sehemu ya tano ya uso wa dunia pamoja na bahari za pembeni kama bahari ya Baltiki na Mediteranea. Hivyo ni bahari kubwa ya pili duniani baada ya Pasifiki. Bila bahari hizi za pembeni eneo lake ni kilometa za mraba 82,400,000.
Beseni yake ina umbo kama "S". Kina ya wastani ni mita 3,332; kina kikubwa katika mfereji wa Puerto Rico kinafikia mita 8,605. Upana wa bahari ni kati ya km 2,648 kati ya Brazil na Liberia hadi km 4,830 kati ya Marekani na Afrika ya Kaskazini.
Mikondo ya Atlantiki inatawala hali ya hewa katika nchi zinazoongozana bahari. Kati ya mikondo hizi ni mkondo wa ghuba la Mexiko kutoka eneo la visiwa vya Karibi ukivuka Atlantiki na kubeba maji ya moto (ambayo bado ni vuguvugu kiasi wakati wa baridi) hadi pwani la Ulaya. Mkondo huu umesababisha ya kwamba sehemu kubwa ya Ulaya ina hali ya hewa ya wastani bila joto au baridi kali mno na mvua nyingi hivyo kuhakikisha rutuba ya bara. Bandari za Ulaya hubaki bila barafu hadi kaskazini kabisa.