Yohane Mbatizaji Chon Changun (alifariki Nei-Ko-Ri, 9 Machi 1866) alikuwa baba wa nyumbani aliyefanya utume kwa kubatiza watu na kuchapa vitabu vya Kikristo pamoja na Petro Choe Hyong. Kwa ajili hiyo waliteswa sana, lakini walidumu katika imani kwa kuvumilia yote kiasi cha kushangaza watesi wao [1].
Ni kati ya kundi kubwa la Wakristo wa Kanisa Katoliki nchini Korea waliouawa kwa ajili ya imani yao katika miaka 1791–1888. Wanakadiriwa kuwa 8,000 - 10,000.
Yeye na wenzake 102 walitangazwa na Papa Yohane Paulo II kuwa watakatifu tarehe 6 Mei 1984.[2]
Sikukuu ya hao Wafiadini wa Korea huadhimishwa tarehe 20 Septemba, lakini ya kwake mwenyewe tarehe ya kifodini chake[3].
Mwishoni mwa karne ya 18, Ukristo wa Kikatoliki ulianza kuenea taratibu nchini[4] kwa juhudi za wananchi walei. Mwaka 1836 Korea, nchi ya Kikonfusyo ilipata wamisionari wa kwanza kutoka nje (wanashirika wa Paris Foreign Missions Society)[5].
Chini ya nasaba ya Joseon, Ukristo ulifutwa, tena waamini walidhulumiwa na kuuawa. Waliobaki walipaswa kushika imani yao kwa siri.