Jina la Kigiriki Byzantion liliendelea kutumika kama jina badala ya Konstantinopoli mara kwa mara na kuwa chanzo cha "Ufalme wa Bizanti" jinsi sehemu ya mashariki ya Dola la Roma ilivyoitwa baada ya mwisho wa utawala wa Kiroma katika magharibi. [1][2]
Hakuna uhakika kuhusu vyanzo vya Bizanti. Kufuatana na kisa kimoja mji ulianziswa na Byzas, mwana wa mfalme wa Megara iliyokuwepo karibu na Athene. Herodoti alitaja mwaka 667 KK kama mwaka wa kuundwa kwa mji, hivyo miaka 17 baada ya mji wa Kalsedonia uliopo upande mwingine wa mlangobahari wa Bosporus. [4]
Bizanti ilikuwa hasa mji wa biashara kutokana na mahali pake kwenye lango pekee la Bahari Nyeusi. Bizanti baadaye ilivamia Kalsedonia iliyopo kuvukia Bosporus upande wa Asia iliyoendelea kama sehemu ya Bizanti.
Katika karne ya 4 BK, wakati ilipokuwa sehemu ya Dola la Roma, Bizanti iliteuliwa na Kaizari Konstantino I kama mji wake mkuu ikajulikana pia kama "Nova Roma" (Roma Mpya) akiipamba na majengo mengi mazuri. Baadaye jiji hilo liliitwa Konstantinopoli (Kigiriki Κωνσταντινούπολις, Konstantinoupolis, yaani "mji wa Konstantino").