Kati ya miaka 1405 na 1433 Zheng He aliongoza misafara 7 za baharini kama kiongozi wa vikundi vikubwa vya meli. Meli zake zilikuwa majahazi makubwa sana yaliyobeba hadi tani 1500. Kila safari Zheng He alipewa meli 50-60 na idadi ya wanajeshi na mabaharia ilikuwa takriban 25,000 - 30,000.
Safari tatu za kwanza zilipeleleza maeneo yanayoitwa leo Indonesia, Uhindi na Sri Lanka. Katika safari za tatu hadi saba aliendelea hadi pwani za Afrika.
Wataalamu kadhaa wamedai ya kwamba kwenye safari ya 1421kundi dogo la meli zake liliingia Atlantiki na kuivuka hadi kufika Amerika. Lakini hii inapingwa na wataalamu wengi.
Hata hivyo kuna ramani ya dunia ya MwitaliaFra Mauro ya mwaka 1459 aliyechora meli ya Kichina katika Atlantiki pamoja na maelezo ya kwamba yeye alipata habari kuhusu meli kubwa kutoka mashariki iliyoingia Atlantiki. Maelezo yale hayaeleweki kabisa kwa sababu wakati ule Wareno walikuwa hawajafika bado kusini mwa Afrika wala hawakuingia Bahari Hindi bado na Amerika haikujulikana, hivyo Fra Mauro hakuwa na majina kwa yale aliyosikia.
Zheng alikufa ama wakati wa safari yake ya mwisho au mara moja baada ya kurudi akazikwa karibu na mji wa Nanjing.
Mwisho wa safari
Makaisari wa baadaye walisimamisha safari. Mitindo wa Zheng He ilikuwa na gharama kubwa sana. Yote ililipiwa na serikali kuu na gharama zilipita faida ya bidhaa zilizoletwa. Tofauti na safari za Wareno na Wahispania waliofika Amerika, Afrika Mashariki na Uhindi miaka 60 baada ya Zheng He, China haikutafuta faida ya kiuchumi katika upelelezi wake na pia haikutambua nafasi za biashara katika nchi hizo za mbali.
Meli kubwa za Zheng He zilifungwa bandarini zikaoza polepole.
Marejeo
↑J. V. G. Mills (1970). Ying-yai Sheng-lan, The Overall Survey of the Ocean's Shores (1433), translated from the Chinese text edited by Feng Ch'eng Chun with introduction, notes and appendices by J. V. G. Mills. White Lotus Press. uk. 5. ISBN974-8496-78-3.
↑Edward L. Dreyer (2007). Zheng He: China and the Oceans in the Early Ming, 1405–1433. Longman. uk. 12. ISBN0-321-08443-8.
↑Tsai, Shih-shan Henry. "Zheng He." World Book Student. World Book, 2013. 4 December 2013.