Mkoa wa Mtwara

Mahali pa Mkoa wa Mtwara katika Tanzania
Mikindani Bay

Mtwara ni jina la mji na mkoa wa Tanzania wenye postikodi namba 63000.

Mkoa wa Mtwara ni kati ya mikoa 31 ya Tanzania. Uko katika pembe ya kusini-mashariki kabisa la nchi. Umepakana na Mkoa wa Lindi upande wa kaskazini, Bahari Hindi kwa mashariki, Msumbiji katika kusini na Mkoa wa Ruvuma upande wa magharibi. Mpaka wa kusini ni Mto Ruvuma.

Ukiwa na km² 16,720 Mtwara ni mkoa mdogo katika Tanzania pamoja na Kilimanjaro.

Wakazi

Jumla kuna wakazi 1,634,947 waishio humo kadiri ya sensa ya mwaka 2022[1] (kutoka 1,270,854 wa sensa ya mwaka 2012)[2].

Wanawake wanazidi wakiwa asilimia 53 ya wakazi wote kwa sababu wanaume wengi hutoka nje kutafuta kazi.

Kati ya makabila ya Mtwara ndio Wamakonde wanaojulikana zaidi kutokana na sanaa yao ya uchongaji wa ubao, hasa mpingo.

Utawala

Kuna wilaya 9: Mtwara Mjini (pia iliitwa "Mikindani"), Mtwara Vijijini, Masasi Mjini, Masasi, Nanyamba, Nanyumbu, Newala Mjini, Newala na Tandahimba.

Ndani yake kuna tarafa 21, kata 98 na vijiji 554.

Uchumi

Mtwara iko kati ya mikoa iliyobaki nyuma miaka mingi kutokana na ugumu wa mawasiliano na barabara isiyopitika kwa sehemu kubwa ya kila mwaka.

Historia ya Mtwara inakuja sambamba na kumbukumbu la jaribio la Waingereza la kuanzisha mradi mkubwa wa maendeleo katika eneo hili ulioshindikana kabisa.

Kuanzia mwaka 1947 serikali ya kikoloni ilijenga bandari ya Mtwara pamoja na reli. Vilevile Mtwara mjini ilipangwa vizuri na kubwa. Sababu yake ilikuwa mpango wa kuanzisha kilimo cha mashamba makubwa kwa ajili ya karanga hasa zilizohitajika kwa ajili ya mahitaji ya Waingereza ya mafuta ya kupikia.

Mradi huo ulishindikana kabisa, pesa nyingi zilipotea hadi mradi ulifutwa kabla ya Tanzania kupata uhuru. Reli iliondolewa tena mwaka 1963.

Bandari imebaki ambayo haijaona kazi nyingi lakini bado ina faida ya kuwa na nafasi nzuri sana ya kupokea meli kubwa. Wakati wa mapambano dhidi ya serikali ya ubaguzi wa rangi katika Afrika Kusini mipango mbalimbali ilitungwa kutengeneza njia ya kupeleka bidhaa kutoka bandari ya Mtwara kwenda Songea na kutoka huko Malawi kwa kuvuka Ziwa Nyasa.

Baada ya kujengwa kwa daraja juu ya mto Rufiji mwaka 2002 kuna matumaini mpya ya kuwa na barabara inayotumika kati ya Mtwara na Dar es Salaam.

Eneo la Mnazi Bay ina gesi inayoweza kutumika kwa mahitaji ya nishati ya eneo lote.

Tegemeo kubwa la uchumi kwa mkoa wa Mtwara ni kilimo, hasa ikitegemea zao la korosho kwa wakulima wa wilaya zote za mkoa.

Kwa miaka ya karibuni wilaya ya Tandahimba na Masasi ndizo zimekuwa wazalishaji wa kiwango cha juu wa korosho. Pia mfumo wa stakabadhi ghalani umesaidia kwa kiasi fulani kwa miaka ya awali ya uanzishwaji mfumo huo (msimu wa 2008/2009) kwa miaka iliyofuata vyama vya msingi vimeonekana kuelemewa na mfumo huo na kusababisha sintofahamu inayoweza kurekebishwa kwa kuwahusisha wadau wote wa zao la korosho.

Majimbo ya bunge

Wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015 mkoa huu ulikuwa na majimbo ya uchaguzi yafuatayo:

Tazama pia

Marejeo

  1. https://www.nbs.go.tz
  2. "Sensa ya 2012, uk. 87, Table 9.0: Population of Mtwara Region" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2016-03-03. Iliwekwa mnamo 2016-05-17.

Viungo vya nje


Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mtwara bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Mkoa wa Mtwara kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.