Ukanda wa mvua hufika kaskazini takriban kama Tropiki ya Kansa na kusini takriban kama Tropiki ya Kaprikoni. Karibu na latitudo hizo kuna msimu mmoja wa mvua na msimu mmoja wa kiangazi kila mwaka. Kwenye ikweta kuna misimu miwili ya mvua na miwili ya kiangazi, wakati ukanda wa mvua hupita mara mbili kwa mwaka, mara moja kuelekea kaskazini na mara moja kuelekea kusini. Kati ya Tropiki na ikweta maeneo yanaweza kukumbwa na msimu mfupi wa mvua (vuli) na msimu mrefu wa mvua (masika) na kiangazi kifupi na kiangazi kirefu. Jiografia ya maeneo mahususi inaweza kurekebisha mifumo hii ya hali ya hewa kwa kiasi kikubwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika Afrika mwanzo wa msimu wa kiangazi unaambatana na kuongezeka kwa visa vya surua na magonjwamengine ya kuambukiza, ambayo watafiti wanaamini huenda yanachangiwa na msongamano mkubwa wa watu wakati wa kiangazi, kwani shughuli za kilimo karibu haiwezekani bila umwagiliaji. Wakati huo baadhi ya wakulima huhamia mijini na hivyo kutengeneza maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu na kuruhusu magonjwa kuenea kwa urahisi zaidi[3].
Utafiti
Data mpya zinaonyesha kuwa katika sehemu za Msitu wa Amazon katika Amerika ya Kusini ukuaji na ufunikaji wa majani hutofautiana kati ya misimu ya kiangazi na ya mvua, na takriban 25% zaidi ya majani na ukuaji wa haraka zaidi wakati wa kiangazi. Watafiti wanaamini kwamba Amazon yenyewe ina athari katika kuleta mwanzo wa msimu wa mvua, kwa sababu kwa kukua majani mengi huvukiza maji zaidi[4]. Walakini, ukuaji huo unaonekana tu katika sehemu zisizo na usumbufu za bonde la Amazon, ambapo watafiti wanaamini kwamba mizizi inaweza kufikia ndani zaidi na kukusanya maji zaidi ya maji ya ardhini[5]. Imeonyeshwa pia kwamba viwango vya ozoni ni vya juu zaidi wakati wa kiangazi kuliko msimu wa mvua katika bonde la Amazon[6].