Vidubini (kwa Kiingereza: microorganism au microbe) ni jina la kundi la viumbehai vidogo sana. Kidubini hakionekani kwa macho bali kwa msaada wa kitambo kama hadubini pekee.
Vidubini ni kundi lenye tabia tofauti sana kati yao. Vingi vyao vina seli moja pekee lakini kuna pia vidubini vyenye seli kadhaa kama vile kuvu na algae. Tabia ya pamoja ni udogo pekee.
Kwa jumla idadi ya vidubini ni kubwa kabisa kuliko viumbehai wote wengine na asilimia 70 za biomasi duniani ni vidubini. Maana yake ni kwamba kwa pamoja viumbe hivi vidogo visivyoonekana kwa macho ni vizito kushinda wanyama na mimea yote ya dunia.
Vidubini ni muhimu katika lishe ya viumbe vingine; vinatekeleza kazi ya kuozesha mata hai iliyokufa (mimea, maiti, mizoga) na kuibadilisha katika hali inayoweza kutumiwa na mimea.
Vidubini vinavyoishi peke yao
Vidubini visivyoishi ndani ya miili ya viumbehai wengine vinapata nishati yao kwa njia mbalimbali.
Vingi hutumia nishati ya nuru kwa njia ya usanisinuru, sawa na mimea. Vingine vinatumia kemikali asilia katika mazingira yao na vikitumia nishati inayopatikana kwa kuvunja muungo kemia wa kampaundi.
Vingine vinaishi kwa kuozesha mata hai iliyokufa kama majani yaliyoanguka, maiti na mizoga ya wanyama. Katika mazingira asilia mata iliyooza inachanganywa tena na udongo na hivyo kwa njia hii vinarudisha virutubishi katika ardhi ambavyo vingepungua mno bila mchakato wa kuoza na kurudisha virutubisho.
Vidubini vingi vinapatikana ndani ya viumbehai wengine na kupata nishati yao kutokana na lishe ya viumbehai hao au kutokana na miili yao.
Hasa vidubini ndani ya utumbo vinasaidia kumega vyakula na kutoa virutubisho kwa ajili ya miili yetu.[5]
Vingine ni pathojeni vinavyosababisha magonjwa ya kuambukiza kwa sababu vinaongezeka ndani ya mwili na kupita kutoka mtu mmoja kwa mtu mwingine. Kuoza kwa meno kunasababishwa na bakteria zinazokula sukari mdomoni na kutoa asidi inayoharibu gamba la jino.
Inawezekana kujikinga kwa kutunza chakula vizuri, kusafisha meno na mikono na kuepukana kuwa karibu sana na baadhi ya wagonjwa.
Marejeo
↑Rybicki E.P. 1990. The classification of organisms at the edge of life, or problems with virus systematics. S African J Sci. 86: 182–6. {{cite journal}}: Missing or empty |title= (help)CS1 maint: numeric names: authors list (link)
↑Lwoff A. 1957. The concept of virus. J. Gen. Microbiol. 17 (2): 239–53. PMID13481308. {{cite journal}}: Missing or empty |title= (help)CS1 maint: numeric names: authors list (link)
↑Forterre P. 2010. Defining life: the virus viewpoint. Orig Life Evol Biosph. 40(2):151-60. [1]
↑Dinorah Pous (2003). Blue Planet. McGrawHill. {{cite book}}: Cite has empty unknown parameter: |coauthors= (help)
BBC News, 28 September, 2001: The microbes that 'rule the world' Citat: "... The Earth's climate may be dependent upon microbes that eat rock beneath the sea floor, according to new research....The number of the worm-like tracks in the rocks diminishes with depth; at 300 metres (985 feet) below the sea floor, they become much rarer..."
Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kidubini kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.