Hakuunda familia yake, bali alibaki kapera bila kuoa akafa mwaka 1625.
Kazi
Bayer amekuwa maarufu kwa atlasi yake ya nyota ya Uranometria ("Uranometria Omnium Asterismorum" - "Ramani ya anga ya makundinyota yote") iliyochapishwa mara ya kwanza mjini Augsburg mwaka 1603.
Hii ilikuwa atlasi ya kwanza ya nyota yenye ramani 51: moja-moja kwa ajili ya kila kundinyota lilojulikana tangu zamani za Ptolemaio ukurasa unaoonyesha kundinyota mpya kwenye nusutufe ya kusini zilizobuniwa na Petrus Plancius na ramani mbili za angakusi na angakaskazi. Kila ramani ina alama za kuonyesha longitudo na latitudo alizochukua kutoka orodha ya nyota ya Tycho Brahe ambayo haikuchapishwa bado wakati wa kutolewa kwa Uranometria.
Bayer alitumia kazi ya Tycho Brahe, inawezekana alitumia pia atlasi ya nyota ya Alessandro Piccolomini ya mwaka 1540 ingawa Bayer aliongeza zaidi ya nyota 1,000 kwa orodha za watangulizi wake.
Katika kitabu cha Uranometria alianzisha mfumo mpya wa kutaja nyota inayojulikana kama "majina ya Bayer". Humo alipanga kila nyota katika kundinyota fulani. Ndani ya kundinyota aliipa kila nyota herufi ya Kigiriki kufuatana na uangavu: nyota angavu zaidi iliitwa Alfa, iliyofuata Beta, halafu Gamma na kadhalika.
Katika atlasi yake aliingiza makundinyota 12 mpya zilizobuniwa miaka michache iliyopita kutaja nyota za angakusi ambazo hazikujulikana na wataalamu wa Ugiriki ya Kale na Roma ya Kale.[3]