Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni mkono muhimu na wenye nguvu wa Umoja wa Mataifa. Baraza la Usalama linajadili masuala ya usalama na amani kati ya mataifa na kuwa na madaraka ya kutoa maazimio.
Baraza la Usalama lilikuwa na mkutano wake wa kwanza tarehe 17 Januari mwaka 1946 katika jumba la Church House mjini London. Tangu mkutano huo, baraza hilo ambalo halifungi mikutano yake, limesafiri kwa upana, likifanya mikutano katika miji mingi, kama vile Paris na Addis Ababa, ila kwa kawaida katika makao yake makuu katika jumba la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Wanachama
Kuna wanachama 15 wa Baraza la Usalama. Kati ya hao watano ni wanachama wa kudumu na 10 ni wanachama wa kuchaguliwa ambao si wa kudumu wenye vipindi vya miaka miwili.
Mpangilio msingi umeelezwa katika Sura ya V ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Ni lazima wajumbe wa Baraza la Usalama wawe daima katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York ili Baraza la Usalama liweze kukutana wakati wowote. Jambo hili la Mkataba wa Umoja wa Mataifa limepangwa kwa makusudi kwa sababu Shirikisho la Mataifa lilishindwa mara nyingi kutatua shida za dharura.
Nguvu za baraza zinafafanuliwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa: ni kama vile kuanzisha vikwazo vya kiuchumi, kuanzisha operesheni ya kudumisha amani na kuruhusu hatua za kijeshi.
Kama nchi inatenda kwa njia isiyokubalika Baraza la Usalama lina mamlaka ya kutoa tamko dhidi ya nchi husika.
Mifano:
Mwaka 2005 Baraza liliamua ya kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ifanye utafiti kama mauaji ya kimbari au hatia dhidi ya ubinadamu zimetokea katika Darfur; kutokana na azimio hili rais wa Sudan ameshtakiwa.
Baraza liliona ya kwamba Uajemi haitekelezi wajibu wake kuhusu miradi ya nyuklia, kwa hiyo nchi zote na watu wote wanakataliwa kuiuzia Uajemi au kupeleka huko bidhaa zinazofaa kwa shughuli za nyuklia.
Mwaka 2011 Baraza liliamua kuzuia usafiri kwa ndege juu ya Libya na kuwapa wanachama haki ya kuchukua hatua za kijeshi kwa kulinda raia dhidi ya mashambulizi kutoka serikali ya nchi hii.
Veto
Nchi 5 ambazo ni wanachama wa kudumu zina haki ya kutamka turufu (kwa Kilatiniveto, "nakataza") yaani kila moja inaweza kuzuia azimio lolote la baraza.
Mara nyingi nchi wanachama wa kudumu wanatumia veto yao kwa kuzuia maazimio dhidi ya nchi fulani kama wenyewe wanaona sababu ya kulinda nchi ile. Hivyo China imetumia veto kuzuia maazimo dhidi ya nchi kama Sudan au Myanmar; Marekani inatumia veto yake mara kwa mara kwa maazimio dhidi ya Israel; nchi zote 5 zinazuia maazimio yanayokwenda kinyume na siasa yao wenyewe.
Azimo la Baraza la Usalama wakati wa vita ya Korea kuingilia kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini iliwezekana tu kwa sababu Umoja wa Kisovyeti iliyopinga hatua hii haikuhudhuria mikutano kwa kipindi cha miezi 8 katika mwaka 1950.